Matendo ya Mitume. Chapter 22

1 Enyi wanaume, ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni, nikijitetea mbele yenu sasa.
2 Waliposikia kwamba anasema nao kwa lugha ya Kiebrania wakazidi kunyamaza; akasema,
3 Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;
4 nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake.
5 Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
6 Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote.
7 Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?
8 Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi.
9 Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami.
10 Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye.
11 Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski.
12 Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko,
13 Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.
14 Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake.
15 Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.
16 Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.
17 Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho,
18 nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu.
19 Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi.
20 Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua.
21 Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa.
22 Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi.
23 Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu,
24 yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii.
25 Hata walipokwisha kumfunga kwa kamba, Paulo akamwambia yule akida aliyesimama karibu, Je! Ni halali ninyi kumpiga mtu aliye Mrumi naye hajakuhumiwa bado?
26 Yule akida aliposikia, akaenda akamwarifu yule jemadari, akisema, Unataka kufanya nini? Kwa maana mtu huyu ni Mrumi.
27 Jemadari akaja, akamwuliza, Niambie, u Mrumi? Akasema, Ndiyo.
28 Jemadari akajibu, Mimi nalipata wenyeji huu kwa mali nyingi. Paulo akasema, Na mimi ni Mrumi wa kuzaliwa.
29 Basi wale waliokuwa tayari kumwuliza wakaondoka wakamwacha. Na yule jemadari naye akaogopa, alipojua ya kuwa ni Mrumi, na kwa sababu amemfunga.
30 Siku ya pili yake akitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao.