Mhubiri. Chapter 2

1 Nikauambia moyo wangu, Haya, nitakujaribu kwa njia ya furaha basi ujifurahishe kwa anasa. Na tazama, hayo nayo yakawa ubatili.
2 Nikasema juu ya kicheko, Ni wazimu; na juu ya furaha, Yafaa nini?
3 Moyoni mwangu nikapeleleza jinsi ya kuuburudisha mwili kwa mvinyo, na (moyo wangu ukali ukiniongoza kwa hekima) jinsi ya kushikana na upumbavu, hata niyaone yaliyo mema ya kuwafaa wanadamu, ili wayafanye hayo chini ya mbingu siku zote za maisha yao.
4 Nikajifanyizia kazi zilizo kubwa; nikajijengea nyumba; nikajipandia mashamba ya mizabibu;
5 nikajifanyizia bustani na viunga, na kuipanda humo miti yenye matunda ya kila namna;
6 nikajifanyizia birika za maji, ya kuunyweshea mwitu mlimopandwa miti michanga.
7 Nami nikanunua watumwa na wajakazi, nikawa na wazalia nyumbani mwangu; tena nikawa na mali nyingi za ng'ombe na kondoo, kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu;
8 tena nikajikusanyia fedha na dhahabu, na tunu za kifalme na za kutoka katika majimbo. Nikajipatia waimbaji, waume kwa wake, nao wale ambao wanadamu wanawatunuka, masuria wengi sana.
9 Basi nikawa mkuu, nikaongezeka kupita wote walionitangulia katika Yerusalemu; pia hekima yangu nikakaa nayo.
10 Wala sikuyanyima macho yangu cho chote yalichokitamani; wala sikuuzuia moyo wangu katika furaha yo yote; maana moyo wangu ulifurahi kwa sababu ya kazi yangu yote, na hii ilikuwa sehemu yangu katika kazi yangu yote.
11 Kisha nikaziangalia kazi zote zilizofanywa kwa mikono yangu, na taabu yote niliyotaabika katika kuzitenda; na tazama, yote ni ubatili na kujilisha upepo, wala faida hakuna chini ya jua.
12 Nikageuka ili kuipambanua hekima, na wazimu na upumbavu. Kwa maana mtu amfuataye mfalme afanye nini? Lilo hilo tu lililokwisha kufanywa.
13 Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza;
14 macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa.
15 Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
16 Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu!
17 Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.
18 Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata.
19 Naye ni nani ajuaye kama huyo atakuwa mwenye hekima au mpumbavu? Hata hivyo atatawala juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo, ambamo ndani yake mimi nimeonyesha hekima chini ya jua. Hayo nayo ni ubatili.
20 Kwa hiyo nikageuka kukata tamaa moyoni mwangu juu ya kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua.
21 Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu.
22 Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua?
23 Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili.
24 Mwanadamu hapati jema kupita kula na kunywa, na kuiburudisha roho yake kwa mema katika kazi yake. Hayo nayo naliona ya kwamba hutoka mkononi mwa Mungu.
25 Kwa maana ni nani awezaye kula au kujiburudisha kuliko mimi?
26 Kwa sababu Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha; bali mkosaji humpa taabu, ili kukusanya na kututa, apate kumpa huyo ambaye Mungu amridhia. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.