Esta. Chapter 8

1 Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu.
2 Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani.
3 Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi.
4 Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme.
5 Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme.
6 Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu?
7 Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi.
8 Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua.
9 Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao.
10 Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia muhuri kwa pete ya mfalme, akazipeleka barua kwa matarishi, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme.
11 Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu Wayahudi wakusanyike katika kila mji na kuzisimamia maisha zao, kuangamiza, na kuua, na kulifisha jeshi lote la watu na la jimbo watakaowaondokea, wao na wadogo wao na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara;
12 siku moja, katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.
13 Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao.
14 Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni.
15 Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia.
16 Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi.
17 Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia.