Mwanzo. Chapter 18
1 Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.
2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,
3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.
4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.
5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.
6 Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate.
7 Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa.
8 Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala.
9 Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani.
10 Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake.
11 Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake.
12 Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee?
13 Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee?
14 Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.
15 Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka.
16 Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize.
17 Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo,
18 akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa?
19 Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.
20 Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana,
21 basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua.
22 Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana.
23 Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu?
24 Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo?
25 Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki?
26 Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.
27 Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu.
28 Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano.
29 Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini.
30 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini.
31 Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini.
32 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi.
33 Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.