Mwanzo. Chapter 46
1 Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye.
2 Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa.
3 Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko.
4 Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako.
5 Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua.
6 Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye.
7 Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri.
8 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe: Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.
9 Na wana wa Reubeni; Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi.
10 Na wana wa Simeoni; Yemueli na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli, mwana wa mwanamke Mkanaani.
11 Na wana wa Lawi; Gershoni, na Kohathi, na Merari.
12 Na wana wa Yuda; Eri, na Onani, na Shela, na Peresi, na Zera; lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani. Na wana wa Peresi, ni Hesroni, na Hamuli.
13 Na wana wa Isakari; Tola, na Puva, na Yashubu, na Shimroni.
14 Na wana wa Zabuloni; Seredi, na Eloni, na Yaleeli.
15 Hao ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo katika Padan-aramu, na Dina, binti yake. Nafsi zote za wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.
16 Na wana wa Gadi; Sefoni, na Hagi, na Shuni, na Esboni, na Eri, na Arodi, na Areli.
17 Na wana wa Asheri; Imna, na Ishva, na Ishvi, na Beria, na Sera, umbu lao. Na wana wa Beria ni Heberi, na Malkieli.
18 Hao ndio wana wa Zilpa, ambaye Labani alimpa Lea, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao, nafsi kumi na sita.
19 Wana wa Raheli, mkewe Yakobo Yusufu na Benyamini.
20 Walizaliwa kwake Yusufu katika nchi ya Misri, Manase na Efraimu, aliomzalia Asenathi binti Potifera, kuhani wa Oni.
21 Na wana wa Benyamini; Bela, na Bekeri, na Ashbeli, na Gera, na Naamani, na Ehi, na Roshi, na Mupimu, na Hupimu, na Ardi.
22 Hao ndio wana wa Raheli, aliomzalia Yakobo, nafsi zote walikuwa kumi na wanne.
23 Na wana wa Dani; Hushimu.
24 Na wana wa Naftali; Yaseeli, na Guni, na Yaseri, na Shilemu.
25 Hao ndio wana wa Bilha, ambaye Labani alimpa Raheli, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao; nafsi zote walikuwa saba.
26 Nafsi zote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri waliotoka viunoni mwake, bila wake za wanawe Yakobo, nafsi zote walikuwa sitini na sita.
27 Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa nafsi wawili. Nafsi zote za nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini.
28 Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni.
29 Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kizima.
30 Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.
31 Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia.
32 Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo.
33 Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini?
34 Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.