Mwanzo. Chapter 33
1 Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao.
2 Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho.
3 Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake.
4 Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia.
5 Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake.
6 Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama.
7 Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama.
8 Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu.
9 Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako.
10 Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami.
11 Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea.
12 Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia.
13 Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng'ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote.
14 Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri.
15 Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu.
16 Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri.
17 Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi.
18 Yakobo akaja kwa amani mpaka mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji.
19 Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha.
20 Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli.