Hosea. Chapter 10
1 Israeli ni mzabibu, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri.
2 Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao.
3 Yakini sasa watasema, Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi Bwana; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini?
4 Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.
5 Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-Aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka.
6 Nayo itachukuliwa Ashuru, iwe zawadi kwa mfalme Yarebu; Efraimu atapata aibu, na Israeli atalionea haya shauri lake mwenyewe.
7 Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji.
8 Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni.
9 Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; ili vita vilivyokuwa juu ya wana wa uovu visiwapate katika Gibea.
10 Wakati nitakapopenda nitawaadhibu; na hao mataifa watakusanyika juu yao, watakapofungwa kwa sababu ya makosa yao mawili.
11 Naye Efraimu ni ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; lakini nimepitisha kongwa juu ya shingo yake nzuri; nitampandisha mwenye kupanda juu ya Efraimu; Yuda atalima, na Yakobo atavunja madongoa yake.
12 Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta Bwana, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.
13 Mmelima dhuluma, mmevuna uovu; mmekula matunda ya uongo; kwa maana uliitumainia njia yako, na wingi wa mashujaa wako.
14 Kwa sababu hiyo fitina itatokea kati ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa, kama vile Shalmani alivyoharibu Betharbeli, katika siku ya vita; mama akavunjika-vunjika pamoja na watoto wake.
15 Hivyo ndivyo Betheli atakavyowatenda ninyi, kwa sababu ya ubaya wenu mwingi; wakati wa mapambazuko mfalme wa Israeli atakatiliwa mbali kabisa.