Yeremia. Chapter 12

1 Wewe u mwenye haki, Ee Bwana, nitetapo nawe, lakini nitasema nawe katika habari ya haki. Mbona njia ya wabaya inasitawi? Mbona wote watendao hila wanakaa salama?
2 Umewapanda, naam, wametia mizizi, wanakua, naam, wanazaa matunda; katika vinywa vyao u karibu, bali katika mioyo yao u mbali.
3 Lakini wewe, Bwana, wanijua; umeniona, umeujaribu moyo wangu, jinsi unavyokuelekea; uwakokote kama kondoo waendao kuchinjwa, ukawaweke tayari kwa siku ya kuchinjwa.
4 Hata lini itaomboleza nchi, na kukauka majani ya nchi yote? Kwa ajili ya mabaya yao wakaao ndani yake, wanyama wameangamia na ndege pia; kwa sababu walisema, Hatauona mwisho wetu.
5 Ikiwa umepiga mbio pamoja na hao waendao kwa miguu, nao wamekuchosha, basi wawezaje kushindana na farasi? Na ujapokuwa katika nchi ya amani u salama, lakini utafanyaje hapo katika kiburi cha Yordani?
6 Kwa maana hata ndugu zako, na nyumba ya baba yako, wamekutenda mambo ya hila; naam, wamepiga kelele nyuma yako; usiwasadiki, wajapokuambia maneno mazuri.
7 Nimeiacha nyumba yangu, nimeutupa urithi wangu; nimemtia mpenzi wangu katika mikono ya adui zake.
8 Urithi wangu umekuwa kwangu kama simba msituni; ameinua sauti yake juu yangu; kwa sababu hiyo nimemchukia.
9 Je! Urithi wangu umekuwa kwangu kama ndege mwenye madoadoa? Ndege wakali wanamtulia pande zote? Enendeni, wakusanyeni pamoja wanyama wote wa mwituni, waleteni ili wale.
10 Wachungaji wengi wameliharibu shamba langu la mizabibu, wamelikanyaga fungu langu chini ya miguu yao, wamefanya fungu langu zuri kuwa jangwa la ukiwa.
11 Wamelifanya kuwa ukiwa, na kwa kuwa ni ukiwa linanililia; nchi yote imefanywa kuwa ukiwa, kwa sababu hapana mtu aliyeweka haya moyoni mwake.
12 Watekao nyara wamepanda juu ya vilele vya milima katika nyika; kwa maana upanga wa Bwana utakula toka upande mmoja wa nchi hata upande wa pili wa nchi; hapana mwenye mwili atakayekuwa na amani.
13 Wamepanda ngano, lakini watavuna miiba; wamejiumiza nafsi zao, lakini hawatakuwa na faida; naam, tahayarini kwa ajili ya matunda yenu, kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
14 Bwana asema hivi juu ya jirani zangu wote walio wabaya, waugusao urithi wangu niliowarithisha watu wangu Israeli, Tazama, nitawang'oa katika nchi yao, nami nitaing'oa nyumba ya Yuda isiwe kati yao.
15 Tena itakuwa, baada ya kuwang'oa, nitarudi na kuwahurumia; nami nitawaleta tena, kila mtu aingie katika urithi wake, na kila mtu aingie katika nchi yake.
16 Kisha itakuwa, ikiwa watajifunza kwa bidii njia za watu wangu, kuapa kwa jina langu, Kama Bwana aishivyo, vile vile kama walivyowafundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watakapojengwa kati ya watu wangu.
17 Bali, kama hawataki kusikia, kung'oa nitaling'oa taifa lile, na kuliangamiza kabisa, asema Bwana.