Ayubu. Chapter 16
1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2 Nimesikia maneno mengi mfano wa hayo; Ninyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha.
3 Je! Maneno yasiyo faida yatakuwa na mwisho? Au, kuna nini kinachokukasirisha, hata ukajibu?
4 Mimi nami ningeweza kunena kama ninyi; Kama roho zenu zingekuwa mahali pa roho yangu, Ningeweza kutunga maneno juu yenu, Na kuwatikisia ninyi kichwa changu.
5 Lakini ningewatia nguvu kwa kinywa changu, Na utuzo wa midomo yangu ungetuliza.
6 Nijapokuwa nanena, huzuni yangu haitulizwi; Nijapokuwa najizuia, nimepunguziwa kitu gani?
7 Lakini sasa amenichokesha; Jamii yangu yote umeifanya ukiwa.
8 Umenishika sana, ni ushahidi juu yangu; Na kukonda kwangu kwaniinukia, kwanishuhudia usoni pangu.
9 Amenirarua katika ghadhabu zake, na kunionea; Amesaga-saga meno juu yangu; Mtesi wangu hunikazia macho makali.
10 Wamenifumbulia vinywa vyao; Wamenipiga shavuni kwa kunitukana; Hujikutanisha pamoja juu yangu.
11 Mungu amenitia kwa hao wapotovu, Na kunitupa mikononi mwao waovu.
12 Nilikuwa katika raha, naye akanivunja-vunja; Naam, amenishika shingo, na kuniponda; Tena amenisimamisha niwe shabaha yake.
13 Wapigaji wake wa mishale hunizingira kotekote, Hunipasua viuno vyangu, asinihurumie; Nyonga zangu amezimwaga juu ya nchi.
14 Hunivunja kwa uvunjifu juu ya uvunjifu; Hunishambulia mfano wa jitu shujaa.
15 Nimeshona nguo ya magunia juu ya mwili wangu, Na pembe yangu nimeidhili uvumbini.
16 Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu li katika kope zangu;
17 Ijapokuwa hapana jeuri mikononi mwangu, Na kuomba kwangu ni safi.
18 Ee nchi, usiifunike damu yangu, Na kilio changu kisipate mahali pa kupumzika.
19 Hata sasa, tazama, shahidi wangu yuko mbinguni. Na huyo atakayenidhamini yuko juu.
20 Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia Mungu machozi;
21 Laiti angemtolea mtu hoja mbele ya Mungu, Amtetee na mwanadamu mbele ya jirani yake.
22 Kwani ikiisha pita miaka michache, Nitakwenda njia hiyo ambayo sitarudi tena.