Yohana. Chapter 1

1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.
3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.
4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.
5 Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza.
6 Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.
7 Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye.
8 Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.
9 Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu.
10 Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.
11 Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.
12 Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.
14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
15 Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.
16 Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.
17 Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.
18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
19 Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani?
20 Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo.
21 Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La.
22 Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako?
23 Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya.
24 Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo.
25 Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule?
26 Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi.
27 Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.
28 Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza.
29 Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!
30 Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.
31 Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji.
32 Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.
33 Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.
34 Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
35 Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake.
36 Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!
37 Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu.
38 Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?
39 Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi.
40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu.
41 Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo).
42 Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).
43 Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate.
44 Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro.
45 Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.
46 Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.
47 Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.
48 Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.
49 Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.
50 Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.
51 Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.