Yohana. Chapter 12

1 Basi, siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu.
2 Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumikia; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye.
3 Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu.
4 Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema,
5 Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini?
6 Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo.
7 Basi Yesu alisema, Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu.
8 Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote.
9 Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu.
10 Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye;
11 maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.
12 Nayo siku ya pili yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu;
13 wakatwaa matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli!
14 Naye Yesu alikuwa amepata mwana-punda, akampanda, kama vile iliyoandikwa,
15 Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.
16 Mambo hayo wanafunzi wake hawakuyafahamu hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kwamba ameandikiwa hayo, na ya kwamba walimtendea hayo.
17 Basi wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua.
18 Na kwa sababu hiyo mkutano walikwenda kumlaki, kwa kuwa wamesikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo.
19 Basi Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lo lote; tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake.
20 Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.
21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.
22 Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.
23 Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.
24 Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
25 Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
26 Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
27 Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.
29 Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye.
30 Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
31 Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.
33 Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa.
34 Basi mkutano wakamjibu, Sisi tumesikia katika torati ya kwamba Kristo adumu hata milele; nawe wasemaje ya kwamba imempasa Mwana wa Adamu kuinuliwa? Huyu Mwana wa Adamu ni nani?
35 Basi Yesu akawaambia, Nuru ingaliko pamoja nanyi muda kidogo. Enendeni maadamu mnayo nuru hiyo, giza lisije likawaweza; maana aendaye gizani hajui aendako.
36 Maadamu mnayo nuru, iaminini nuru hiyo, ili mpate kuwa wana wa nuru. Hayo aliyasema Yesu, akaenda zake, akajificha wasimwone.
37 Walakini ajapokuwa amefanya ishara nyingi namna hiyo mbele yao, hawakumwamini;
38 ili litimie lile neno la nabii Isaya alilolisema, Bwana, ni nani aliyezisadiki habari zetu; Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani?
39 Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena,
40 Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.
41 Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake.
42 Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.
43 Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.
44 Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka.
45 Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka.
46 Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani.
47 Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu.
48 Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.
49 Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema.
50 Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.