Mambo ya Walawi. Chapter 4
1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Haya, nena na wana wa Israeli, uwaambie, Kama mtu ye yote akifanya dhambi pasipo kukusudia, katika neno lo lote ambalo Bwana amelizuilia lisifanywe, na kutenda neno lo lote la maneno hayo;
3 kama kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi, hata analeta hatia juu ya watu; ndipo na atoe kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya, na kumsongeza kwa Bwana ng'ombe mume mchanga mkamilifu, kuwa ni sadaka ya dhambi.
4 Naye atamleta huyo ng'ombe na kumweka mlangoni pa hiyo hema ya kukutania, mbele za Bwana; naye ataweka mkono wake kichwani mwake ng'ombe, na kumchinja huyo ng'ombe mbele za Bwana.
5 Kisha huyo kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa baadhi ya damu ya huyo ng'ombe, na kuileta ndani ya hiyo hema ya kukutania;
6 kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza damu mbele ya Bwana mara saba, mbele ya pazia la mahali patakatifu.
7 Kisha kuhani atatia baadhi ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba mzuri mbele ya Bwana iliyo ndani ya hema ya kukutania; kisha damu yote ya huyo ng'ombe ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyoko mlangoni pa hema ya kukutania.
8 Kisha mafuta yote ya huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi atayaondoa; mafuta yote yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
9 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo, hayo yote atayaondoa,
10 vile vile kama yanavyoondolewa katika ng'ombe wa kuchinjwa kwa sadaka za amani; kisha huyo kuhani atayateketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
11 Kisha ngozi yake ng'ombe, na nyama yake yote, pamoja na kichwa chake, na pamoja na miguu yake, na matumbo yake, na mavi yake,
12 maana, huyo ng'ombe mzima atamchukua nje ya marago hata mahali safi, hapo wamwagapo majivu, naye atamchoma moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo majivu yamwagwapo.
13 Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na Bwana, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia;
14 hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania.
15 Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng'ombe mbele za Bwana;
16 kisha ng'ombe atachinjwa mbele za Bwana. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa katika damu ya huyo ng'ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania;
17 kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za Bwana, mbele ya pazia mara saba.
18 Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za Bwana, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania.
19 Kisha atayaondoa mafuta yake yote na kuyateketeza juu ya madhabahu.
20 Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng'ombe; kama alivyomfanyia huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu vivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa.
21 Kisha atamchukua huyo ng'ombe nje ya marago, na kumchoma moto vile vile kama alivyomchoma moto ng'ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano.
22 Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lo lote katika hayo ambayo Bwana, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia;
23 akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi awe matoleo yake, mume, mkamilifu;
24 kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za Bwana; ni sadaka ya dhambi.
25 Kisha kuhani atatwaa katika damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza.
26 Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.
27 Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lo lote katika hayo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia;
28 akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi mke mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya.
29 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa.
30 Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu.
31 Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.
32 Naye akileta mwana-kondoo kuwa sadaka ya dhambi, ataleta wa kike mkamilifu.
33 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake sadaka ya dhambi, kisha atamchinja awe sadaka ya dhambi, mahali hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa.
34 Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya kuteketezwa kwa kidole chake na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kisha damu yake yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu;
35 kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama mafuta ya mwana-kondoo yalivyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kwa desturi ya hizo sadaka za Bwana zilizosongezwa kwa njia ya moto; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.