Luka. Chapter 1
1 Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,
2 kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,
3 nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,
4 upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.
5 Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.
6 Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.
7 Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.
8 Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,
9 kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.
10 Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.
11 Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.
12 Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
13 Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.
14 Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.
15 Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.
16 Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.
17 Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.
18 Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.
19 Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.
20 Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake.
21 Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni.
22 Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu.
23 Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake.
24 Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema,
25 Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.
26 Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,
27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
28 Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.
29 Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?
30 Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.
31 Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.
32 Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
34 Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?
35 Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.
36 Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa;
37 kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.
38 Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
39 Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,
40 akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.
41 Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu;
42 akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
43 Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?
44 Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.
45 Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.
46 Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
47 Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;
48 Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
49 Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu.
50 Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha.
51 Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
52 Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza.
53 Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
54 Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake;
55 Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele.
56 Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.
57 Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume.
58 Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye.
59 Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria.
60 Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana.
61 Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo.
62 Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita.
63 Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote.
64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu.
65 Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi.
66 Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
67 Na Zakaria, baba yake, akajazwa Roho Mtakatifu, akatabiri, akisema,
68 Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake, na kuwakomboa.
69 Ametusimamishia pembe ya wokovu Katika mlango wa Daudi, mtumishi wake.
70 Kama alivyosema tangu mwanzo Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu;
71 Tuokolewe na adui zetu Na mikononi mwao wote wanaotuchukia;
72 Ili kuwatendea rehema baba zetu, Na kulikumbuka agano lake takatifu;
73 Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
74 Ya kwamba atatujalia sisi, Tuokoke mikononi mwa adui zetu, Na kumwabudu pasipo hofu,
75 Kwa utakatifu na kwa haki Mbele zake siku zetu zote.
76 Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu, Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana umtengenezee njia zake;
77 Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao.
78 Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, Ambazo kwa hizo mwangaza utokao juu umetufikia,
79 Kuwaangaza wakaao katika giza na uvuli wa mauti, Na kuiongoza miguu yetu kwenye njia ya amani.
80 Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.