Malaki

1 Ufunuo wa neno la Bwana kwa Israeli kwa mkono wa Malaki
2 Nimewapenda ninyi, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Umetupendaje? Je! Esau siye ndugu yake Yakobo? Asema Bwana; ila nimempenda Yakobo;
3 bali Esau nimemchukia na kuifanya milima yake kuwa ukiwa, na urithi wake nimewapa mbweha wa nyikani.
4 Ijapokuwa Edomu asema, Tumepondwa-pondwa, lakini tutarudi na kupajenga mahali palipoachwa hali ya ukiwa; Bwana wa majeshi asema hivi, Wao watajenga, bali mimi nitaangusha; na watu watawaita, Mpaka wa uovu, na, Watu ambao Bwana anawaghadhabikia milele.
5 Na macho yenu ninyi yataona, nanyi mtasema, Bwana ndiye mkuu kupita mpaka wa Israeli.
6 Mwana humheshimu baba yake, na mtumishi humcha bwana wake; basi, kama mimi ni baba yenu, heshima yangu iko wapi? Na kama mimi ni bwana wenu, kicho changu ki wapi? Bwana wa majeshi awauliza ninyi, enyi makuhani, mnaolidharau jina langu. Nanyi mwasema, Tumelidharau jina lako kwa jinsi gani?
7 Mnatoa chakula kilichotiwa unajisi juu ya madhabahu yangu Nanyi mwasema, Sisi tumekutia unajisi kwa jinsi gani? Kwa sababu mwasema, Meza ya Bwana ni kitu cha kudharauliwa.
8 Tena mtoapo sadaka aliye kipofu, si vibaya? Na mtoapo sadaka walio vilema na wagonjwa, si vibaya? Haya! Mtolee liwali wako; je! Atakuwa radhi nawe? Au atakukubali nafsi yako? Asema Bwana wa majeshi.
9 Na sasa, nawasihi, ombeni fadhili za Mungu, ili atupe neema; ikiwa jambo hili limetoka katika mikono yenu; je! Atawakubali nafsi zenu? Asema Bwana wa majeshi.
10 Laiti angekuwapo kwenu mtu mmoja wa kuifunga milango; msije mkawasha moto bure madhabahuni pangu! Sina furaha kwenu, asema Bwana wa majeshi, wala sitakubali dhabihu yo yote mikononi mwenu.
11 Kwa maana tokea maawio ya jua hata machweo yake jina langu ni kuu katika Mataifa; na katika kila mahali unatolewa uvumba na dhabihu safi kwa jina langu; maana jina langu ni kuu katika Mataifa, asema Bwana wa majeshi.
12 Lakini ninyi mnalitia unajisi, kwa kuwa mwasema, Meza ya Bwana imetiwa unajisi; na matunda yake, yaani, nyama yake, hudharauliwa.
13 Tena mwasema, Tazama, jambo hili linatuchokesha namna gani! Nanyi mmelidharau, asema Bwana wa majeshi; nanyi mmeleta kitu kilichopatikana kwa udhalimu, na kilema, na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka; je! Niikubali hii mikononi mwenu? Asema Bwana.
14 Lakini na alaaniwe mtu mwenye kudanganya, ambaye katika kundi lake ana mume, akaweka nadhiri, ila amtolea Bwana kitu kilicho na kilema; kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa.