Marko. Chapter 16
1 Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.
2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;
3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi?
4 Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.
5 Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu.
6 Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.
7 Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.
8 Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa. [
9 Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba.
10 Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia.
11 Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki.
12 Baada ya hayo akawatokea watu wawili miongoni mwao, ana sura nyingine; nao walikuwa wakishika njia kwenda shamba.
13 Na hao wakaenda zao wakawapa habari wale wengine; wala hao hawakuwasadiki.
14 Baadaye akaonekana na wale kumi na mmoja walipokuwa wakila, akawakemea kwa kutokuamini kwao na ugumu wa mioyo yao, kwa kuwa hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka katika wafu.
15 Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.
16 Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.
17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
19 Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu.
20 Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.]