Nehemia. Chapter 2

1 Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote.
2 Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.
3 Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?
4 Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.
5 Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.
6 Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda.
7 Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng'ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda;
8 nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.
9 Ndipo nikafika kwa maliwali walio ng'ambo ya Mto, nikawapa hizo nyaraka za mfalme. Naye mfalme alikuwa amepeleka maakida wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami.
10 Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli.
11 Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.
12 Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe.
13 Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto.
14 Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama aliyekuwa chini yangu.
15 Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo.
16 Wala mashehe hawakujua nilikokwenda, wala nilivyotenda; wala sijawaambia Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala mashehe, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo.
17 Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena.
18 Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema.
19 Lakini waliposikia Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Mtaasi ninyi juu ya mfalme?
20 Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu.