1 Mambo ya Nyakati. Chapter 15
1 Basi Daudi akajifanyia nyumba katika mji wa Daudi; akapaweka tayari mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema.
2 Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua Bwana, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima.
3 Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la Bwana, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari.
4 Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi;
5 wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia na ishirini;
6 wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini;
7 wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia na thelathini;
8 wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili;
9 wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini;
10 wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia na kumi na wawili.
11 Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu,
12 akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari.
13 Kwani kwa sababu ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, Bwana, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta sawasawa na sheria.
14 Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli.
15 Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la Bwana.
16 Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha.
17 Basi Walawi wakamwagiza Hemani mwana wa Yoeli; na wa nduguze, Asafu mwana wa Berekia; na wa wana wa Merari ndugu zao, Ethani mwana wa Kishi;
18 na pamoja nao ndugu zao kwa cheo cha pili, Zekaria, na Yaasieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu; na Benaya, na Maaseya, na Matithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, mabawabu.
19 Hivyo hao waimbaji, Hemani, Asafu, na Ethani, wakaagizwa kupiga matoazi yao ya shaba kwa sauti kuu;
20 na Zekaria, na Yaasieli na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu, na Maaseya, na Benaya, wenye vinanda vya sauti ya Alamothi;
21 na Matithiya, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, na Azazia, wenye vinubi vya sauti ya Sheminithi,
22 waongoze. Na Kenania, mkuu wa Walawi, alikuwa juu ya uchukuzi; yeye aliusimamia uchukuzi, kwa sababu alikuwa mstadi.
23 Na Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.
24 Na Shebania, na Yoshafati, na Nethaneli, na Amasai, na Zekaria, na Benaya, na Eliezeri, makuhani, wakapiga baragumu mbele ya sanduku la Mungu; na Obed-edomu na Yehia walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku.
25 Basi Daudi, na wazee wa Israeli, na maakida wa maelfu, wakaenda, ili kulipandisha sanduku la agano la Bwana kutoka nyumbani mwa Obed-edomu kwa furaha kuu;
26 hata ikawa, Mungu alipowajalia Walawi waliolichukua sanduku la agano la Bwana, wakachinja ng'ombe saba, na kondoo waume saba.
27 Naye Daudi alikuwa amevaa joho ya kitani safi, na Walawi wote waliolichukua sanduku, na waimbaji, na Kenania msimamizi wa uchukuzi, na waimbaji; naye Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.
28 Ndivyo Israeli wote walivyolipandisha sanduku la agano la Bwana kwa shangwe na kwa sauti ya tarumbeta, na kwa baragumu, na kwa matoazi, wakipiga sauti kuu kwa vinanda na vinubi.
29 Hata ikawa, sanduku la agano la Bwana lilipofika mjini kwa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi, akicheza na kushangilia; akamdharau moyoni mwake.