1 Mambo ya Nyakati. Chapter 19

1 Ikawa baada ya hayo, Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, akafa, akamiliki mwanawe mahali pake.
2 Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akapeleka wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize.
3 Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Waona Daudi amheshimu babayo kwa kukupelekea wafariji? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuiangalia nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza?
4 Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawakatia nguo zao katikati, hata matakoni, akawatoa waende zao.
5 Wakaenda watu wakamwambia Daudi jinsi walivyotendewa wale watu. Naye akatuma watu kuwalaki; kwa sababu watu hao walikuwa wametahayarika sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hata mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi.
6 Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, Hanuni na wana wa Amoni wakapeleka talanta elfu za fedha ili kujiajiria magari na wapanda farasi kutoka Mesopotamia, na kutoka Atam-maaka, na kutoka Soba.
7 Basi wakajiajiria magari thelathini na mbili elfu, na mfalme wa Maaka na watu wake; nao walikuja wakatua mbele ya Medeba. Na wana wa Amoni wakakusanyika kutoka miji yao, wakaja vitani.
8 Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.
9 Wakatoka wana wa Amoni, wakapanga vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwandani.
10 Basi Yoabu alipoona ya kwamba uso wa vita umekuwa juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami.
11 Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni.
12 Akasema, Wakiwa Washami ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe.
13 Uwe hodari, tukajitie moyo mkuu kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Bwana afanye yaliyo mema machoni pake.
14 Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake.
15 Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu.
16 Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakapeleka wajumbe, wakawavuta Washami walioko ng'ambo ya Mto, na Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza.
17 Alipoambiwa Daudi; akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akawajia, akapanga vita juu yao. Basi Daudi alipopanga vita juu ya Washami, wakapigana naye.
18 Washami wakakimbia mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami watu wa magari saba elfu, na askari waendao kwa miguu arobaini elfu, akamwua na Shobaki, jemadari wa jeshi.
19 Na watumwa wa Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Daudi, wakamtumikia; wala Washami hawakukubali kuwasaidia wana wa Amoni tena.