1 Mambo ya Nyakati. Chapter 13
1 Kisha Daudi akafanya shauri na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, naam, na kila kiongozi.
2 Daudi akawaambia jamii yote ya Israeli, Likiwa jema kwenu, tena likiwa limetoka kwa Bwana, Mungu wetu, na tutume watu huku na huku mahali pote kwa ndugu zetu waliosalia katika nchi yote ya Israeli, ambao pamoja nao makuhani na Walawi wamo ndani ya miji yao yenye viunga, ili wakusanyike kwetu;
3 nasi tujirudishie tena sanduku la Mungu wetu; maana hamkuuliza neno kwa hilo katika siku za Sauli.
4 Nao jamii nzima wakasema ya kwamba watafanya hivyo; kwa kuwa neno hilo lilikuwa jema machoni pa watu wote.
5 Basi Daudi akawakusanya Israeli wote, toka Shihori, kijito cha Misri, hata pa kuingilia Hamathi, ili kwamba walilete sanduku la Mungu kutoka Kiriath-yearimu.
6 Basi Daudi akapanda, yeye na Israeli wote, mpaka Baala, ndio Kiriath-yearimu, ulio wa Yuda, ili kulileta toka huko sanduku la Mungu, Bwana akaaye juu ya makerubi, lililoitwa kwa Jina lake.
7 Wakalipandisha sanduku la Mungu juu ya gari jipya kutoka nyumba ya Abinadabu; na Uza na Ahio wakaliendesha lile gari.
8 Wakacheza Daudi na Israeli wote, mbele za Mungu, kwa nguvu zao zote; na kwa nyimbo na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa matoazi, na kwa tarumbeta.
9 Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe walikunguwaa.
10 Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu.
11 Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo.
12 Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, Nitajileteaje sanduku la Mungu kwangu?
13 Basi Daudi hakujichukulia sanduku mjini mwa Daudi, ila akalihamisha kando na kulitia nyumbani kwa Obed-edomu Mgiti.
14 Sanduku la Mungu likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo.