1 Mambo ya Nyakati. Chapter 29

1 Kisha mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote, Sulemani mwanangu, ambaye Mungu amemchagua peke yake, akali ni mchanga bado na mwororo, nayo kazi hii ni kubwa; kwani nyumba hii ya enzi si kwa mwanadamu, ila kwa Bwana, Mungu.
2 Basi kwa uwezo wangu wote nimeiwekea akiba nyumba ya Mungu wangu, dhahabu kwa vitu vya dhahabu, na fedha kwa vitu vya fedha, na shaba kwa vitu vya shaba, na chuma kwa vitu vya chuma, na miti kwa vitu vya miti; vito vya shohamu, na vya kujazia, vito vya njumu, na vya rangi mbalimbali, na mawe ya thamani ya kila namna, na marimari tele.
3 Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku yangu, nami ninayo hazina yangu mwenyewe ya dhahabu na fedha, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, zaidi ya hiyo akiba niliyoiwekea tayari nyumba takatifu;
4 yaani, talanta elfu tatu za dhahabu, za dhahabu ya Ofiri, na talanta elfu saba za fedha iliyosafika, ya kuzifunikiza kuta za nyumba;
5 ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa Bwana?
6 Ndipo wakuu wa mbari za mababa, na wakuu wa kabila za Israeli, na maakida wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao;
7 nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi,na fedha taranta elfu kumi, na shaba taranta elfu kumi na nane ,na chuma taranta elfu mia.
8 Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya Bwana, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni.
9 Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea Bwana; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu.
10 Kwa hiyo Daudi akamhimidi Bwana, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele.
11 Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote.
12 Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote.
13 Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu.
14 Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea.
15 Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana.
16 Ee Bwana, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe.
17 Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao.
18 Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako;
19 naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba.
20 Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini Bwana, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi Bwana, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia Bwana, na mfalme naye.
21 Wakamtolea Bwana dhabihu, wakamchinjia Bwana sadaka za kuteketezwa, siku ya pili yake, yaani, ng'ombe elfu, na kondoo waume elfu, na wana-kondoo elfu, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote;
22 wakala na kunywa mbele za Bwana siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za Bwana, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani.
23 Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha Bwana, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii.
24 Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakajitia chini ya mfalme Sulemani.
25 Naye Bwana akamtukuza Sulemani mno machoni pa Israeli wote, akampa fahari ya kifalme ya kumpita mfalme awaye yote aliyekuwa kabla yake katika Israeli.
26 Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli wote.
27 Na wakati aliotawala juu ya Israeli, ulikuwa miaka arobaini; miaka saba alitawala Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akatawala Yerusalemu.
28 Akafa mwenye umri mwema, ameshiba siku, na mali, na heshima; naye Sulemani mwanawe akamiliki badala yake.
29 Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo na mwisho, angalia, zimeandikwa katika tarehe ya Samweli, mwonaji, na katika tarehe ya Nathani, nabii, na katika tarehe ya Gadi, mwonaji;
30 pamoja na kutawala kwake kote na nguvu zake, nazo zamani zilizompata yeye, na Israeli, na falme zote za nchi.