1 Wakorintho. Chapter 12

1 Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu.
2 Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa Mataifa, mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa.
3 Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu.
4 Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
5 Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.
6 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
7 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.
8 Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;
9 mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;
10 na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;
11 lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.
12 Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.
13 Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
14 Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.
15 Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?
16 Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?
17 Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?
18 Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.
19 Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
20 Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.
21 Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi.
22 Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi.
23 Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.
24 Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa;
25 ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe.
26 Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.
27 Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.
28 Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.
29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?
30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?
31 Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.