1 Wafalme. Chapter 8
1 Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, wamwendee mfalme Sulemani huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la Bwana kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni.
2 Wakakutana mbele ya mfalme Sulemani watu wote wa Israeli wakati wa sikukuu, katika mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
3 Wazee wote wa Israeli wakaja, nao makuhani wakajitwika sanduku.
4 Wakalipandisha sanduku la Bwana, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwa katika ile Hema; vitu hivyo makuhani na Walawi wakavipandisha.
5 Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli waliokutanika kwake, walikuwako pamoja naye mbele ya sanduku, wakichinja sadaka kondoo na ng'ombe, wasioweza kuhesabiwa wala kufahamiwa idadi yao kwa kuwa wengi.
6 Makuhani wakalileta sanduku la agano la Bwana hata mahali pake, katika chumba cha ndani cha ile nyumba, patakatifu pa patakatifu, naam, chini ya mbawa za makerubi.
7 Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.
8 Na ile miti kwa kuwa mirefu, ncha za miti zilionekana katika mahali patakatifu, mbele ya chumba cha ndani; lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo.
9 Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili za mawe ambazo Musa aliziweka ndani huko Horebu, Bwana alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka katika nchi ya Misri.
10 Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu;
11 hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana.
12 Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene.
13 Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.
14 Mfalme akageuza uso wake, akawabariki mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.
15 Akasema, Bwana, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena na Daudi baba yangu kwa kinywa chake akalitimiza kwa mkono wake, akasema,
16 Tokea siku ile nilipowatoa watu wangu Israeli katika Misri, sikuchagua mji wo wote katika kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe hapo; lakini nalimchagua Daudi awe juu ya watu wangu Israeli.
17 Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
18 Lakini Bwana akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako.
19 Lakini wewe hutanijengea nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
20 Basi Bwana amelitimiza neno lile alilolinena; nami nimesimama mahali pa Daudi baba yangu, na kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli, kama Bwana alivyoahidi, nami nimeijenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli.
21 Na humo sanduku hili nimelifanyizia mahali, ambalo ndani yake mna maagano ya Bwana, aliyoyafanya na baba zetu, hapo alipowatoa katika nchi ya Misri.
22 Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Bwana, machoni pa mkutano wote wa Israeli, akaikunjua mikono yake mbinguni.
23 Akasema Ee Bwana, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe, mbinguni juu wala duniani chini; ushikaye maagano na rehema kwa watumishi wako, waendao mbele zako kwa mioyo yao yote.
24 Umemtimizia mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia; naam, ulinena kwa kinywa chako, ukayatimiza kwa mkono wako, kama ilivyo leo.
25 Na sasa, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, umfikilizie mtumishi wako, Daudi, baba yangu, ahadi uliyomwahidia, ukisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha Israeli machoni pangu, kama watoto wako wakiangalia njia zao, ili kuenenda mbele zangu kama wewe ulivyoenenda.
26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, nakusihi, ulithibitishe neno lako, ulilomwambia mtumishi wako, Daudi, baba yangu.
27 Lakini Mungu je? Atakaa kweli kweli juu ya nchi? Tazama, mbingu hazikutoshi, wala mbingu za mbingu; sembuse nyumba hii niliyoijenga!
28 Walakini uyaelekee maombi ya mtumwa wako, na dua yake, Ee Bwana, Mungu wangu, uisikilize sauti na maombi ya mtumwa wako, aombayo mbele zako leo.
29 Macho yako yafumbuke na kuielekea nyumba hii usiku na mchana, mahali hapa ulipopataja, ukasema, Hapa ndipo litakapokuwapo jina langu; ili uyasikie maombi ya mtumwa wako aombapo akikabili mahali hapa.
30 Uisikie dua ya mtumwa wako, na ya watu wako Israeli, watakapoomba wakikabili mahali hapa; naam, sikia huko mbinguni, makao yako; nawe usikiapo, samehe.
31 Ikiwa mtu amemkosa mwenzake, na kupewa sharti ya kiapo aapishwe, naye akija na kuapa hapa mbele ya madhabahu yako, katika nyumba hii;
32 basi, usikie huko mbinguni, ukatende, ukawahukumu watumwa wako; ukimpatiliza mtu mbaya, kwa kuleta njia yake juu ya kichwa chake; na kumpa mwenye haki haki yake, ukimjalia kwa kadiri ya haki yake.
33 Ikiwa watu wako Israeli wamepigwa mbele ya adui zao, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakirejea tena kwako, na kulikiri jina lako wakikuomba na kukusihi katika nyumba hii;
34 basi, usikie huko mbinguni, ukawaachilie watu wako Israeli dhambi yao, ukawarejeze tena katika nchi uliyowapa baba zao.
35 Ikiwa mbingu zimefungwa, hata hakuna mvua, kwa sababu wamekukosa wewe; kama wakiomba wakikabili mahali hapa, na kulikiri jina lako, na kuiacha dhambi yao, wakati ule utakapowatesa;
36 basi, usikie huko mbinguni, ukaisamehe dhambi ya watumwa wako, na ya watu wako Israeli; unapowafundisha njia iliyo njema, iwapasayo kuiendea; ukanyeshe mvua juu ya nchi yako, uliyowapa watu wako iwe urithi wao.
37 Ikiwa nchi imeingia njaa, au tauni, au ukosefu wa mvua, au ukungu, au nzige, au panzi; ikiwa adui wamewahusuru katika nchi ya miji yao; au ukiwapo msiba wo wote, au uele wo wote;
38 maombi yo yote au dua yo yote ikifanywa na mtu awaye yote, au na watu wako Israeli wote pamoja, watakaojua kila mtu maradhi ya moyo wake, na kuikunjua mikono yake kuielekea nyumba hii;
39 basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukasamehe, ukatende, ukampe kila mtu kwa kadiri ya njia zake; wewe ujuaye moyo wake; (maana wewe peke yako ndiwe uijuaye mioyo ya wanadamu wote);
40 ili wakuche wewe siku zote watakazoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
41 Hata na mgeni naye, asiyekuwa mmoja wa watu wako Israeli, atakapokuja kutoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya jina lako;
42 (maana watasikia habari za jina lako kuu, na za mkono wako ulio hodari, na za mkono wako ulionyoshwa); atakapokuja na kuomba kuielekea nyumba hii;
43 basi, usikie huko mbinguni, makao yako, ukatende kwa kadiri ya yote atakayokuomba mgeni huyo; ili watu wote wa dunia wapate kulijua jina lako, na kukucha wewe kama watu wako Israeli, nao wajue ya kuwa nyumba hii, niliyoijenga, imeitwa kwa jina lako.
44 Ikiwa watu wako watoka kwenda kupigana na adui zao, kwa njia yo yote utakayowapeleka, wakikuomba, Bwana, kuuelekea mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
45 basi, uyasikie huko mbinguni maombi yao na dua yao, ukaitetee haki yao.
46 Ikiwa wamekutenda dhambi, (maana hakuna mtu asiyetenda dhambi), hata ukawaghadhibikia, ukawatia katika mikono ya adui zao, wawachukue mateka mpaka nchi ya adui zao, iliyo mbali au iliyo karibu;
47 basi, wakijirudia nafsi zao katika nchi ile watakayochukuliwa mateka, wakitubu, na kukusihi katika nchi ya hao waliowachukua mateka, wakisema, Tumekosa, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu;
48 watakaporejea kwako kwa mioyo yao yote, na kwa nia zao zote, katika nchi ya adui zao, waliowachukua mateka, wakikuomba, kwa kuikabili nchi yao, uliyowapa baba zao, na mji huu uliouchagua, na nyumba hii niliyoijenga kwa jina lako;
49 basi, uyasikie maombi yao na dua yao, huko mbinguni, makao yako, ukaitetee haki yao;
50 ukawasamehe watu wako waliokutenda dhambi, na makosa yao yote waliyokukosa; ukawape kuonewa huruma mbele yao waliowachukua mateka, ili wapate kuwahurumia.
51 Kwa kuwa ni watu wako, na urithi wako, uliowatoa katika Misri, toka katikati ya tanuu ya chuma.
52 Macho yako na yafumbuke, na kuielekea dua ya mtumwa wako, na dua za watu wako Israeli, ukawasikilize kila wakati watakapokulilia.
53 Kwa maana uliwatenga na watu wote wa dunia, wawe urithi wako, kama ulivyonena kwa mdomo wa Musa, mtumishi wako, hapo ulipowatoa baba zetu katika Misri, Ee Bwana MUNGU.
54 Hata ikawa, Sulemani alipokwisha kumwomba Bwana maombi hayo, na dua hiyo yote, akasimama na kuondoka hapo mbele ya madhabahu ya Bwana, hapo alipokuwa amepiga magoti, na kuikunjua mikono yake kuelekea mbinguni.
55 Akasimama, na kuwabariki mkutano wote wa Israeli kwa sauti kuu, akasema,
56 Na ahimidiwe Bwana, aliyewapa watu wake Israeli kustarehe, vile vile kama yote aliyoyaahidi. Halikukosa kupatikana neno lo lote katika ahadi yake njema, aliyoahidi kwa mkono wa Musa, mtumishi wake.
57 Bwana, Mungu wetu, na akae nasi, kama alivyokaa na baba zetu; asituache, wala asitutupe;
58 aielekeze mioyo yetu kwake, ili tuende katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na sheria zake, na hukumu zake, alizowaamuru baba zetu.
59 Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za Bwana, na yawe karibu na Bwana, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku.
60 Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa Bwana ndiye Mungu; hakuna mwingine.
61 Mioyo yenu na iwe kamili kwa Bwana, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.
62 Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za Bwana.
63 Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea Bwana, ng'ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoifanya wakfu nyumba ya Bwana.
64 Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya Bwana; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za Bwana ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani.
65 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za Bwana, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne.
66 Hata siku ya nane akaagana na watu, nao wakambarikia mfalme, wakaenda hemani kwao, wakifurahi na kuchangamka moyoni kwa wema wote Bwana aliomfanyia Daudi mtumishi wake, na Israeli watu wake.