1 Samweli. Chapter 5
1 Basi Wafilisti walikuwa wamelichukua sanduku la Mungu, wakaenda nalo kutoka Eben-ezeri hata Ashdodi.
2 Wafilisti wakalichukua sanduku la Mungu, wakalitia katika nyumba ya Dagoni, wakaliweka karibu na Dagoni.
3 Na watu wa Ashdodi, walipoamka alfajiri siku ya pili, kumbe! Dagoni imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana. Wakaitwaa Dagoni, wakaisimamisha mahali pake tena.
4 Hata walipoamka kesho yake asubuhi, kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu.
5 Kwa hiyo makuhani wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo.
6 Lakini mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaharibu, akawapiga kwa majipu, huko Ashdodi na mipakani mwake.
7 Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa, walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu.
8 Basi wakatuma watu waende kuwakusanya kwao mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Mungu wa Israeli? Nao wakajibu, Sanduku la Mungu wa Israeli na lihamishwe liende Gathi. Wakalihamisha sanduku la Mungu wa Israeli.
9 Ikawa, walipokwisha lihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa juu ya mji huo, kwa kuwafadhaisha sana; akawapiga watu wa mjini, wadogo kwa wakubwa, wakapatwa na majipu.
10 Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu mpaka Ekroni. Ikawa, sanduku la Mungu lilipofika Ekroni, watu wa Ekroni walifanya kelele, wakasema, Wamelileta hilo sanduku la Mungu wa Israeli kwetu, hata kutuua sisi na watu wetu.
11 Kwa hiyo wakatuma watu waende kuwakusanya mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Liondoeni hilo sanduku la Mungu wa Israeli, liende tena mahali pake, ili lisituue sisi, wala watu wetu; kwa sababu kulikuwa na fadhaa kubwa sana mjini mwote; mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko.
12 Na wale wasiokufa walipigwa kwa yale majipu; na kilio cha mji kikafika mbinguni.