1 Samweli. Chapter 3
1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.
2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),
3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;
4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.
5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.
6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.
7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.
9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.
10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.
11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.
12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.
13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.
14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.
15 Naye Samweli akalala hata asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya Bwana. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo.
16 Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa.
17 Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lo lote katika hayo yote Bwana aliyosema nawe.
18 Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lo lote. Naye akasema, Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema.
19 Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini.
20 Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana.
21 Naye Bwana akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa Bwana akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la Bwana. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.