Zaburi

1 Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
2 Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
3 Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.
4 Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
5 Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki.
6 Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.