Zaburi. Chapter 89

1 Fadhili za Bwana nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
2 Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
3 Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
4 Wazao wako nitawafanya imara milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.
5 Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
6 Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana? Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa malaika?
7 Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka.
8 Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka.
9 Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.
10 Ndiwe uliyemseta Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao.
11 Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake.
12 Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako.
13 Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kuume umetukuka.
14 Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako.
15 Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
16 Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa.
17 Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka.
18 Maana ngao yetu ina Bwana, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.
19 Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi, Ukasema, nimempa aliye hodari msaada; Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu.
20 Nimemwona Daudi, mtumishi wangu, Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
21 Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake, Na mkono wangu utamtia nguvu.
22 Adui hatamwonea, Wala mwana wa uovu hatamtesa.
23 Bali nitawaponda watesi wake mbele yake, Nitawapiga wanaomchukia.
24 Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo, Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.
25 Nitaweka mkono wake juu ya bahari, Na mkono wake wa kuume juu ya mito.
26 Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
27 Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
28 Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu litafanyika amini kwake.
29 Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.
30 Wanawe wakiiacha sheria yangu, Wasiende katika hukumu zangu,
31 Wakizihalifu amri zangu, Wasiyashike maagizo yangu,
32 Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo, Na uovu wao kwa mapigo.
33 Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye, Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo.
34 Mimi sitalihalifu agano langu, Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.
35 Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu, Hakika sitamwambia Daudi uongo,
36 Wazao wake watadumu milele, Na kiti chake kitakuwa kama jua mbele zangu.
37 Kitathibitika milele kama mwezi; Shahidi aliye mbinguni mwaminifu.
38 Walakini Wewe umemtupa na kumkataa, Umemghadhibikia masihi wako.
39 Umechukizwa na agano la mtumishi wako, Umeinajisi taji yake na kuitupa chini.
40 Umeyabomoa maboma yake yote, Umezifanya ngome zake kuwa magofu.
41 Wote wapitao njiani wanateka mali zake; Amekuwa laumu kwa jirani zake;
42 Umeutukuza mkono wa kuume wa watesi wake; Umewafurahisha wote wanaomchukia.
43 Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake; Wala hukumsimamisha vitani.
44 Umeikomesha fahari yake; Kiti chake cha enzi umekitupa chini.
45 Umezipunguza siku za ujana wake; Umemvika aibu.
46 Ee Bwana, hata lini? Utajificha hata milele? Ghadhabu yako itawaka kama moto?
47 Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu; Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu!
48 Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti, Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?
49 Bwana, zi wapi fadhili zako za kwanza, Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako?
50 Ee Bwana, ukumbuke, Wanavyosimangwa watumishi wako; Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu Masimango ya watu wengi.
51 Ambayo adui zako wamesimanga, Ee Bwana, Naam, wamezisimanga hatua za masihi wako.
52 Na ahimidiwe Bwana milele. Amina na Amina.