Zaburi. Chapter 59
1 Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami.
2 Uniponye nao wafanyao maovu, Uniokoe na watu wa damu.
3 Kwa maana wanaiotea nafsi yangu; Wenye nguvu wamenikusanyikia; Ee Bwana, si kwa kosa langu, Wala si kwa hatia yangu.
4 Bila kosa langu huenda mbio, hujiweka tayari; Uamke uonane nami, na kutazama.
5 Na Wewe, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, uamke. Uwapatilize mataifa yote; Usiwarehemu waovu wafanyao uovu hata mmoja.
6 Wakati wa jioni hurudi, hulia kama mbwa, Na kuzunguka-zunguka mjini.
7 Tazama, kwa vinywa vyao huteuka, Midomoni mwao mna panga, Kwa maana ni nani asikiaye?
8 Na Wewe, Bwana, utawacheka, Utawadhihaki mataifa yote.
9 Ee nguvu zangu, nitakungoja Wewe, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu
10 Mungu wa fadhili zangu atanitangulia, Mungu atanijalia kuwatazama adui zangu.
11 Usiwaue, watu wangu wasije wakasahau; Uwatawanye kwa uweza wako, Na kuwaangamiza, Ee Bwana, ngao yetu.
12 Kwa dhambi ya kinywa chao, Na kwa neno la midomo yao, Wanaswe kwa kiburi chao, Kwa ajili ya kulaani na uongo wasemao.
13 Uwakomeshe kwa hasira, Uwakomeshe watoweke, Wajue ya kuwa Mungu atawala katika Yakobo, Na hata miisho ya dunia.
14 Wakati wa jioni hurudi, hulia kama mbwa, Na kuzunguka-zunguka mjini.
15 Watatanga-tanga hao wakitafuta chakula; Wasiposhiba watakesha usiku kucha.
16 Nami nitaziimba nguvu zako asubuhi, Nitaziimba fadhili zako kwa furaha. Kwa kuwa ndiwe uliyekuwa ngome yangu, Na makimbilio siku ya shida yangu.
17 Ee nguvu zangu, nitakuimbia kwa furaha, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu, Mungu wa fadhili zangu.