Zaburi. Chapter 49
1 Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani.
2 Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja.
3 Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara.
4 Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi
5 Kwa nini niogope siku za uovu, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
6 Wa hao wanaozitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao;
7 Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake,
8 (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;)
9 ili aishi sikuzote asilione kaburi.
10 Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao.
11 Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Hao waliotaja mashamba yao Kwa majina yao wenyewe.
12 Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao.
13 Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao.
14 Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu.
15 Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha.
16 Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi.
17 Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata.
18 Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema,
19 Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele.
20 Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.