Zaburi. Chapter 108
1 Ee Mungu, moyo wangu u thabiti, Nitaimba, nitaimba zaburi, Naam, kwa utukufu wangu.
2 Amka, kinanda na kinubi, Nitaamka alfajiri.
3 Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu, Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
4 Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni, Na uaminifu wako hata mawinguni.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako.
6 Ili wapenzi wako waopolewe, Uokoe kwa mkono wako wa kuume, uniitikie.
7 Mungu amenena kwa utakatifu wake, Nami nitashangilia. Nitaigawanya Shekemu, Nitalipima bonde la Sukothi.
8 Gileadi ni yangu, na Manase ni yangu, Na Efraimu ni nguvu ya kichwa changu. Yuda ni fimbo yangu ya kifalme,
9 Moabu ni bakuli langu la kunawia. Nitamtupia Edomu kiatu changu, Na kumpigia Filisti kelele za vita.
10 Ni nani atakayenipeleka hata mji wenye boma? Ni nani atakayeniongoza hata Edomu?
11 Ee Mungu, si Wewe uliyetutupa? Wala, Ee Mungu, hutoki na majeshi yetu?
12 Utuletee msaada juu ya mtesi, Maana wokovu wa binadamu haufai.
13 Kwa msaada wa Mungu tutatenda makuu, Maana Yeye atawakanyaga watesi wetu.