Zaburi. Chapter 106
1 Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.
2 Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana, Kuzihubiri sifa zake zote?
3 Heri washikao hukumu, Na kutenda haki sikuzote.
4 Ee Bwana, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. Unijilie kwa wokovu wako,
5 Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako.
6 Tumetenda dhambi pamoja na baba zetu, Tumetenda maovu, tumefanya ubaya.
7 Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu.
8 Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu.
9 Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda.
10 Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao.
11 Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao.
12 Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake.
13 Wakayasahau matendo yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake.
14 Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani.
15 Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao.
16 Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa Bwana.
17 Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu.
18 Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya.
19 Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
20 Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani.
21 Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri.
22 Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
23 Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.
24 Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake.
25 Bali wakanung'unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya Bwana.
26 Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani,
27 Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali.
28 Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu.
29 Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia.
30 Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa.
31 Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele.
32 Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao,
33 Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.
34 Hawakuwaharibu watu wa nchi Kama Bwana alivyowaambia;
35 Bali walijichanganya na mataifa, Wakajifunza matendo yao.
36 Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao.
37 Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani.
38 Wakamwaga damu isiyo na hatia, Damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu.
39 Ndivyo walivyotiwa uchafu kwa kazi zao, Wakafanya uasherati kwa matendo yao.
40 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya watu wake, Akauchukia urithi wake.
41 Akawatia mikononi mwa mataifa, Nao waliowachukia wakawatawala.
42 Adui zao wakawaonea, Wakatiishwa chini ya mkono wao.
43 Mara nyingi aliwaponya, Bali walikuwa wakimwasi kwa mashauri yao, Wakadhilika katika uovu wao.
44 Lakini aliyaangalia mateso yao, Aliposikia kilio chao.
45 Akawakumbukia agano lake; Akawahurumia kwa wingi wa fadhili zake;
46 Akawajalia kuhurumiwa Na watu wote waliowateka.
47 Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe, Utukusanye kwa kututoa katika mataifa, Tulishukuru jina lako takatifu, Tuzifanyie shangwe sifa zako.
48 Na ahimidiwe Bwana, Mungu wa Israeli, Tangu milele hata milele. Watu wote na waseme, Amina. Haleluya.