Zaburi. Chapter 139
1 Ee Bwana, umenichunguza na kunijua.
2 Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
3 Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, Umeelewa na njia zangu zote.
4 Maana hamna neno ulimini mwangu Usilolijua kabisa, Bwana.
5 Umenizingira nyuma na mbele, Ukaniwekea mkono wako.
6 Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.
7 Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako?
8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari;
10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.
11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;
12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.
13 Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
14 Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana,
15 Mifupa yangu haikusitirika kwako, Nilipoumbwa kwa siri, Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi;
16 Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado.
17 Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake!
18 Kama ningezihesabu ni nyingi kuliko mchanga; Niamkapo nikali pamoja nawe.
19 Ee Mungu, laiti ungewafisha waovu! Enyi watu wa damu, ondokeni kwangu;
20 Kwa maana wakuasi kwa ubaya, Adui zako wakutaja jina lako bure.
21 Je! Bwana nisiwachukie wanaokuchukia? Nisikirihike nao wakuasio?
22 Nawachukia kwa ukomo wa chuki, Wamekuwa adui kwangu.
23 Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu;
24 Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.