Zaburi. Chapter 94
1 Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze,
2 Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao.
3 Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?
4 Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi?
5 Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako;
6 Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima.
7 Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.
8 Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili?
9 Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?
10 Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue?
11 Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.
12 Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako;
13 Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.
14 Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake,
15 Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.
16 Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu?
17 Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya.
18 Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza.
19 Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu.
20 Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria?
21 Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia.
22 Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia.
23 Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza.