Zaburi. Chapter 65
1 Ee Mungu, sifa zakulaiki katika Sayuni, Na kwako Wewe itaondolewa nadhiri.
2 Wewe usikiaye kuomba, Wote wenye mwili watakujia.
3 Ingawa maovu mengi yanamshinda, Wewe utayafunika maasi yetu.
4 Heri mtu yule umchaguaye, Na kumkaribisha akae nyuani mwako. Na tushibe wema wa nyumba yako, Patakatifu pa hekalu lako.
5 Kwa mambo ya kutisha utatujibu, Katika haki, Ee Mungu wa wokovu wetu. Wewe uliye tumaini la miisho yote ya dunia, Na la bahari iliyo mbali sana,
6 Milima waiweka imara kwa nguvu zako, Huku ukijifunga uweza kama mshipi.
7 Wautuliza uvumi wa bahari, Uvumi wa mawimbi yake, Na ghasia ya mataifa;
8 Kwa hiyo wakaao mbali kabisa huogopa ishara zako; Milango ya asubuhi na jioni waifurahisha.
9 Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi.
10 Matuta yake wayajaza maji; Wapasawazisha palipoinuka, Wailainisha nchi kwa manyunyu; Waibariki mimea yake.
11 Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono.
12 Huyadondokea malisho ya nyikani, Na vilima vyajifunga furaha.
13 Na malisho yamevikwa kondoo, Na mabonde yamepambwa nafaka, Yanashangilia, naam, yanaimba.