Zaburi. Chapter 63
1 Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, Nafsi yangu inakuonea kiu, Mwili wangu wakuonea shauku, Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.
2 Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu, Nizione nguvu zako na utukufu wako.
3 Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu.
4 Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.
5 Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono; Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.
6 Ninapokukumbuka kitandani mwangu, Nakutafakari Wewe makesha yote ya usiku.
7 Maana Wewe umekuwa msaada wangu, Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.
8 Nafsi yangu inakuandama sana; Mkono wako wa kuume unanitegemeza.
9 Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiharibu, Wataingia pande za nchi zilizo chini.
10 Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga, Watakuwa riziki za mbwa-mwitu.
11 Bali mfalme atamfurahia Mungu, Kila aapaye kwa Yeye atashangilia, Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.