Zaburi. Chapter 36
1 Kuasi kwake yule mwovu hunena moyoni mwake, Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yake.
2 Kwa maana hujipendekeza machoni pake Kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa.
3 Maneno ya kinywa chake ni uovu na hila, Ameacha kuwa na akili na kutenda mema.
4 Huwaza maovu kitandani pake, Hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii.
5 Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni, Uaminifu wako hata mawinguni.
6 Haki yako ni kama milima ya Mungu, Hukumu zako ni vilindi vikuu, Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.
7 Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhili zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.
8 Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako, Nawe utawanywesha mto wa furaha zako.
9 Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru.
10 Uwadumishie wakujuao fadhili zako, Na wanyofu wa moyo uaminifu wako.
11 Mguu wa kiburi usinikaribie, Wala mkono wa wasio haki usinifukuze.
12 Huko ndiko walikoanguka wafanyao maovu; Wameangushwa chini wasiweze kusimama.