Ufunuo wa Yohana. Chapter 15

1 Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia.
2 Tena nikaona kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto, na wale wenye kushinda, watokao kwa yule mnyama, na sanamu yake, na kwa hesabu ya jina lake, walikuwa wamesimama kando-kando ya hiyo bahari ya kioo, wenye vinubi vya Mungu.
3 Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa.
4 Ni nani asiyekucha, Ee Bwana, na kulitukuza jina lako? Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa.
5 Na baada ya hayo nikaona, na hekalu la hema ya ushuhuda mbinguni lilifunguliwa;
6 na wale malaika saba, wenye mapigo saba, wakatoka katika hekalu, wamevikwa mavazi ya kitani safi, ya kung'aa, wamefungwa vifuani mwao mishipi ya dhahabu.
7 Na mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba vitasa saba vya dhahabu, vimejaa ghadhabu ya Mungu, aliye hai hata milele na milele.
8 Hekalu likajazwa moshi uliotoka kwenye utukufu wa Mungu na uweza wake. Wala hapakuwa na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu, hata yatimizwe mapigo saba ya wale malaika saba.