Ufunuo wa Yohana. Chapter 21
1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.
2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.
3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.
4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.
5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.
6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.
7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.
9 Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.
10 Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu;
11 wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri;
12 ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli.
13 Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu.
14 Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
15 Na yeye aliyesema nami alikuwa na mwanzi wa dhahabu, apate kuupima huo mji, na milango yake, na ukuta wake.
16 Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa.
17 Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne, kwa kipimo cha kibinadamu, maana yake, cha malaika.
18 Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi.
19 Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna. Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi;
20 wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso; wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto.
21 Na ile milango kumi na miwili ni lulu kumi na mbili; kila mlango ni lulu moja. Na njia ya mji ni dhahabu safi kama kioo kiangavu.
22 Nami sikuona hekalu ndani yake; kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake.
23 Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwana-Kondoo.
24 Na mataifa watatembea katika nuru yake. Na wafalme wa nchi huleta utukufu wao ndani yake.
25 Na milango yake haitafungwa kamwe mchana; kwa maana humo hamna usiku.
26 Nao wataleta utukufu na heshima ya mataifa ndani yake.
27 Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.