Wimbo Ulio Bora. Chapter 1

1 Wimbo ulio bora, wa Sulemani.
2 Kubusu na anibusu kwa kinywa chake. Maana pambaja zako zapita divai;
3 Manukato yako yanukia vizuri; Jina lako ni kama marhamu iliyomiminwa; Kwa hiyo wanawali hukupenda.
4 Nivute nyuma yako, na tukimbie; Mfalme ameniingiza vyumbani mwake. Tutafurahi na kukushangilia; Tutazinena pambaja zako kuliko divai; Ndiyo, ina haki wakupende.
5 Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri, Enyi binti za Yerusalemu, Mfano wa hema za Kedari, Kama mapazia yake Sulemani.
6 Msinichunguze kwa kuwa ni mweusi-mweusi, Kwa sababu jua limeniunguza. Wana wa mamangu walinikasirikia, Waliniweka niwe mlinzi wa mashamba ya mizabibu; Bali shamba langu mwenyewe sikulilinda.
7 Nijulishe, ee mpendwa wa nafsi yangu, Ni wapi utakapolisha kundi lako, Ni wapi utakapolilaza adhuhuri. Kwa nini niwe kama aliyefungiwa kidoto, Karibu na makundi ya wenzako?
8 Usipojua, wewe uliye mzuri katika wanawake, Shika njia uzifuate nyayo za kondoo, Na kuwalisha wana-mbuzi wako Karibu na hema za wachungaji.
9 Mpenzi wangu, nimekulinganisha Na farasi katika magari ya Farao.
10 Mashavu yako ni mazuri kwa mashada, Shingo yako kwa mikufu ya vito.
11 Tutakufanyizia mashada ya dhahabu, Yenye vifungo vya fedha.
12 Muda mfalme alipoketi juu ya matakia, Nardo yangu ilitoa harufu yake.
13 Mpendwa wangu ni kama mfuko wa manemane Ukilazwa usiku maziwani mwangu.
14 Mpendwa wangu ni kama kishada cha hina, Katika mizabibu huko Engedi.
15 Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua.
16 Tazama, u mzuri, mpendwa wangu, Wapendeza, na kitanda chetu ni majani;
17 Nguzo za nyumba yetu ni mierezi, Na viguzo vyetu ni miberoshi.