Wimbo Ulio Bora. Chapter 7
1 Siti msharifu, jinsi zilivyo nzuri Hatua zako katika mitalawanda. Mapaja yako ya mviringo ni kama johari, Kazi ya mikono ya fundi mstadi;
2 Kitovu chako ni kama bilauri iliyoviringana, Na isikose divai iliyochanganyika; Tumbo lako ni mfano wa chungu ya ngano, Iliyozungukwa na ugo wa nyinyoro;
3 Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Ambao ni mapacha ya paa;
4 Shingo yako ni kama huo mnara wa pembe; Macho yako kama viziwa vya Heshboni, Karibu na mlango wa Beth-rabi; Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni, Unaoelekea Dameski;
5 Kichwa chako juu yako ni kama Karmeli, Na nywele za kichwa chako kama urujuani, Mfalme amenaswa na mashungu yake.
6 Jinsi yalivyo mazuri, yalivyo matamu, Mapenzi katikati ya anasa!
7 Kimo chako kimefanana na mtende, Na maziwa yako na vichala.
8 Nilisema, Nitapanda huo mtende, Na kuyashika makuti yake. Maziwa yako na yawe kama vichala vya mzabibu, Na harufu ya pumzi yako kama mapera;
9 Na kinywa chako kama divai iliyo bora, Kwa mpendwa wangu inashuka taratibu, Ikitiririka midomoni mwao walalao.
10 Mimi ni wake mpendwa wangu, Na shauku yake ni juu yangu.
11 Njoo, mpendwa wangu, twende mashambani, Tufanye maskani katika vijiji.
12 Twende mapema hata mashamba ya mizabibu, Tuone kama mzabihu umechanua, Na maua yake yamefunuka; Kama mikomamanga imetoa maua; Huko nitakupa pambaja zangu.
13 Mitunguja hutoa harufu yake; Juu ya milango yetu yako matunda mazuri, Mapya na ya kale, ya kila namna, Niliyokuwekea, mpendwa wangu.