Wimbo Ulio Bora. Chapter 6
1 Mpendwa wako amekwenda wapi, Wewe uliye mzuri katika wanawake? Mpendwa wako amegeukia upande upi, Ili tumtafute pamoja nawe?
2 Mpendwa wangu ameshukia bustani yake, Kwenye matuta ya rihani; Ili kulisha penye bustani, Ili kuchuma nyinyoro.
3 Mimi ni wake mpendwa wangu, naye ni wangu, Hulisha kundi lake penye nyinyoro.
4 Mpenzi wangu, u mzuri kama Tirza, Mwenye kupendeza kama Yerusalemu, Wa kutisha kama wenye bendera.
5 Uyageuzie macho yako mbali nami, Kwa maana yamenitisha sana. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa Gileadi.
6 Meno yako kama kundi la kondoo, Wakipanda kutoka kuoshwa; Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati yao.
7 Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako.
8 Wako malkia sitini, na masuria themanini, Na wanawali wasiohesabika;
9 Hua wangu, mkamilifu wangu, ni mmoja tu, Mtoto wa pekee wa mamaye. Ndiye kipenzi chake aliyemzaa, Binti wakamwona wakamwita heri; Malkia na masuria nao wakamwona, Wakamsifu, wakisema,
10 Ni nani huyu atazamaye kama alfajiri, Mzuri kama mwezi, safi kama jua, Wa kutisha kama wenye bendera?
11 Nalishukia bustani ya milozi, Ili kuyatazama machipuko ya bondeni; Nione kama mzabibu umechanua, Kama mikomamanga imetoa maua.
12 Kabla sijajua, roho yangu ilinileta Katikati ya magari ya wakuu wangu.
13 Rudi, rudi, Mshulami, Rudi, rudi, ili sisi tukutazame.