Wimbo Ulio Bora. Chapter 3
1 Usiku kitandani nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nalimtafuta, nisimpate.
2 Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate.
3 Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu?
4 Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu; Nikamshika, nisimwache tena, Hata nilipomleta nyumbani mwa mamangu, Chumbani mwake aliyenizaa.
5 Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe.
6 Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani, Mfano wake ni nguzo za moshi; Afukizwa manemane na ubani, Na mavumbi ya manukato yote ya mchuuzi?
7 Tazama, ni machela yake Sulemani; Mashujaa sitini waizunguka, Wa mashujaa wa Israeli.
8 Wote wameshika upanga, Wamehitimu kupigana; Kila mtu anao upanga wake pajani Kwa hofu ya kamsa za usiku.
9 Mfalme Sulemani alijifanyizia machela Ya miti ya Lebanoni;
10 Nguzo zake alizifanyiza za fedha, Na mgongo wake wa dhahabu, Kiti chake kimepambwa urujuani, Gari lake limenakishiwa njumu, Hiba ya binti za Yerusalemu.
11 Tokeni, enyi binti za Sayuni, Mtazameni Mfalme Sulemani, Amevaa taji alivyovikwa na mamaye, Siku ya maposo yake, Siku ya furaha ya moyo wake.