Tito. Chapter 1

1 Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa;
2 katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;
3 akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu;
4 kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.
5 Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;
6 ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii.
7 Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno ,kwa kuwa ni wakili wa MUNGU;asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake,asiwe mwepesi wa hasira,asiwe mlevi wala mgomvi,asiwe mpenda mapato ya aibu.
8 bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake;
9 akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.
10 Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao.
11 Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu.
12 Mtu wa kwao, nabii wao wenyewe, amesema, Wakrete ni waongo siku zote, hayawani wabaya, walafi wavivu.
13 Ushuhuda huo ni kweli. Kwa sababu hiyo uwakemee kwa ukali, ili wapate kuwa wazima katika imani;
14 wasisikilize hadithi za Kiyahudi, wala maagizo ya watu wajiepushao na yaliyo kweli.
15 Vitu vyote ni safi kwa hao walio safi; lakini hakuna kilicho safi kwao walio wanajisi, wasioamini; bali akili zao zimekuwa najisi, na nia zao pia.
16 Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai.