2 Mambo ya Nyakati. Chapter 19

1 Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani.
2 Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao Bwana? Kwa ajili ya hayo ghadhabu i juu yako itokayo kwa Bwana.
3 Walakini yameonekana mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu.
4 Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao.
5 Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji;
6 akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu.
7 Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.
8 Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu.
9 Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili.
10 Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.
11 Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema