Zekaria. Chapter 4

1 Na yule malaika aliyesema nami akanijia mara ya pili, akaniamsha, kama mtu aamshwavyo katika usingizi wake.
2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikasema, Nimeona, na tazama, kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake, na taa zake saba juu yake; tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwa taa zote zilizo juu yake;
3 na mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume walile bakuli, na mmoja upande wake wa kushoto.
4 Nami nikajibu, nikamwambia yule malaika aliyesema nami, nikasema, Ee Bwana wangu, vitu hivi ni nini?
5 Ndipo malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, Hujui vitu hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.
6 Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.
7 Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.
8 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
9 Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu.
10 Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote.
11 Ndipo nikajibu, nikamwambia, Ni nini mizeituni hii miwili iliyo upande wa kuume wa kinara cha taa kile na upande wake wa kushoto?
12 Nami nikajibu mara ya pili, nikamwuliza, Ni nini haya matawi mawili ya mizeituni, ambayo kwa njia ya ile mifereji miwili ya dhahabu hutoa mafuta yao?
13 Akanijibu, akasema, Hujui hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.
14 Ndipo akasema, Hivi ni hao wana wawili wa mafuta, wasimamao karibu na Bwana wa dunia yote.