Zekaria. Chapter 14
1 Tazama, siku moja ya Bwana inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako.
2 Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali.
3 Hapo ndipo atakapotokea Bwana, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita.
4 Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.
5 Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku za Uzia, mfalme wa Yuda; na Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.
6 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;
7 lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na Bwana; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru.
8 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba maji yaliyo hai yatatoka katika Yerusalemu; nusu yake itakwenda upande wa bahari ya mashariki, na nusu yake upande wa bahari ya magharibi; wakati wa hari na wakati wa baridi itakuwa hivi.
9 Naye Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa mmoja, na jina lake moja.
10 Nchi yote itageuzwa kuwa kama Araba, toka Geba mpaka Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu; naye atainuliwa juu, atakaa mahali pake mwenyewe, toka lango la Benyamini mpaka mahali pa lango la kwanza, mpaka lango la pembeni; tena toka mnara wa Hananeli mpaka mashinikizo ya mfalme.
11 Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena; lakini Yerusalemu utakaa salama.
12 Na hii ndiyo tauni, ambayo Bwana atawapiga watu wote waliofanya vita juu ya Yerusalemu; nyama ya mwili wao itaharibika, wasimamapo juu ya miguu yao, na macho yao yataharibika ndani ya vichwa vyao, na ndimi zao zitaharibika vinywani mwao.
13 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba mashaka makubwa yatokayo kwa Bwana yatakuwa kati yao; na kila mmoja wao atakamata mkono wa jirani yake, na mkono wake utainuliwa ili kushindana na mkono wa jirani yake.
14 Yuda naye atafanya vita juu ya Yerusalemu; na huo utajiri wa mataifa wa pande zote utakusanyika, dhahabu, na fedha, na mavazi; vitu vingi sana.
15 Na hivyo ndivyo itakavyokuwa tauni ya farasi, na nyumbu, na ngamia, na punda, na ya hao wanyama wote watakaokuwamo matuoni mle, kama tauni hiyo.
16 Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, na kuishika sikukuu ya Vibanda.
17 Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, mvua haitanyesha kwao.
18 Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo Bwana atawapiga mataifa, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.
19 Hii ndiyo adhabu ya Misri, na adhabu ya mataifa yote, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.
20 Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA Bwana; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya Bwana vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu.
21 Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa Bwana wa majeshi; nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake; wala siku hiyo hatakuwamo tena mfanya biashara ndani ya nyumba ya Bwana wa majeshi.